Polisi wameanzisha uchunguzi baada ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Laikipia kudungwa kwa kisu mara kadhaa na kuaga dunia, huku aliyetekeleza kitendo hicho akijaribu kujitoa uhai kwa kujikata koo pia.
Gertrude Chepkoech ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza alishambuliwa jana na mwanamume anayedaiwa kuwa mpenzi wa rafikiye wanayeishi pamoja.
Mwanamume huyo aliyetambuliwa kwa jina Ezra ambaye ni mwanabodaboda, alijidunga kisu tumboni na kujikata koo katika juhudi za kujaribu kujitoa uhai baada ya umati kutaka kumuua.
Mwanamume huyo hatimaye aliokolewa na maafisa wa polisi na yuko katika hali dhabiti kulingana na madaktari kwenye hospitali kuu ya Nyahururu.
Mwanamume huyo alikuwa amezuiwa na wasimamizi wa chumba hicho kuingia humo baada ya mpenzi wake kudai kwamba alitaka kuingia chumbani mwao kwa nguvu.
Msichana huyo alikuwa peke yake chumbani kwani mwenzake ambaye ni mpenzi wa mshukiwa alikuwa amekwenda kufanya mtihani.
Mwili wa msichana huyo unahifadhiwa katika makafani ya hospitali kuu ya Nyahururu huku uchunguzi kuhusu kisa hicho ukianzishwa
Leave a Comment