Vifo ambavyo vinachangiwa na ajali za piki piki aina ya boda boda vimeendelea kuongezeka na kuhatarisha maisha ya wahudumu pamoja na wateja wao nchini, NTSA imesema.
Kulingana na msimamizi wa mamlaka hiyo ya usafiri na usalama barabarani jimbo la Nakuru Eric Otieno, zaidi ya watu 600 walipoteza maisha yao mwaka jana 2018 kutokana na ajali za boda boda.
Akiongea mjini Molo kaunti ya Nakuru mnamo Jumamosi, Otieno alisema zaidi ya asilimia 50 ya wahudumu wa bodaboda hawajatimiza masharti yaliyowekwa idara ya trafiki, jambo linaloendelea kuweka maisha yao hatarini.
“Data tulio nayo inaonyesha kwamba ajali za pikipiki zimeongezeka kutoka thelathini na nne kutoka mwaka wa 2006, hadi watu wasiopungua 600 kipindi cha mwaka wa 2017/18,” Otieno akasema
Kutokana na hilo afisa huyo alitaka wahudumu wa boda boda kupata mafunzo rasmi ya kuziendesha pikipiki, kuvalia kofia wakiwa kazini na pia kutii sheria za trafiki.
Afisa huyo wa NTSA ameongeza kusema, “Mwaka wa 2006 watu wengi nchini hawakuwa wamekumbatia usafiri wa pikipiki kama ilivyo kwa sasa. Lakini tunawaomba wanaboda boda watii sheria za barabarani ili wawe salama.”
Na Bernard Waweru
Leave a Comment