Wakaazi wa Laikipia sasa wanataka serikali kutatua pia tatizo la uhasama kati ya wanyama pori na binadamu sambamba na matatizo ya usalama.
Hii ni baada ya mfugaji mmoja kupatikana akiwa ameuawa na simba alipokuwa malishoni katika kijiji cha Lekiji, eneo la Laikipia Mashariki.
Mwili wa kijana, Tereua Yiangale (18), ulipatikana na mpita njia mmoja mida ya asubuhi karibu na eneo la Mlima Fisi.
Kulingana na mwenyekiti wa Nyumba Kumi katika kijiji cha Lekiji Resian Shembele, marehemu alikuwa safarini kupeleka kondoo wake malishoni katika kijiji jirani cha Endana akiwa ametoka Ilmotiok alipokumbana na kifo chake.
Ndugu wa marehemu ambaye pia ni chifu wa kijiji cha Ilmotiok, Jacob Yiangele, alisema kuwa kaka yake alishambuliwa mida ya saa kumi alfajiri ya jana Alhamisi, kwani alikuwa akiwalisha kondoo wake mia tatu usiku kucha.
Kulingana na afisa mkuu wa KWS katika eneo la Laikipia Rose Malenya, eneo kati ya ranchi ya Mpala na mbuga ya Oljogi ambapo mhasiriwa alishambuliwa panajulikana kuwa na wanyama pori hatari.
Leave a Comment