News/Habari

Martha karua aendelea kusistiza kwamba hamtambui Rais William Ruto kama Rais wa Kenya

Written by admin

Kinara wa chama cha NARC Martha Karua ambaye pia alikuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais kupitia tikiti ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya amesisitiza msimamo wake kuwa hawezi kumtambua William Ruto kama rais wa Kenya.

Katika moja ya mazungumzo ya kipekee na kituo kimoja cha redio humu nchini, Karua alisema kwamba katu hawezi kushrutishwa kumkubali Ruto kama rais wakati fikira zake zinamueleza kwamba rais hakushinda kwa njia halali.

Mtangazaji alipomuuliza swali la kutaka kujua ni kwa nini kwa mara kadhaa katika mahojiano hayo alikuwa anamtaja Ruto kama naibu rais mstaafu na wala si rais na ndipo alijibu kwamba hawezi kulazimishwa kubadili fikira na mawazo yake kuhusu kile anahisi kilitokea katika uchaguzi wa Agosti 9.

Aidha kiongozi huyo wa muda mrefu anayejulikana kwa misimamo mkali  alizidi kujitetea kwa kusema kwamba huo ndio uamuzi wake kibinafsi na  wala hapatatokea mtu kumbadili kifikira.

Alidokeza kwamba mpango wake wa kuendelea kusukuma ili kupata ukweli na haki katika mahakama ya ukanda wa Afrika Mashariki bado utaendelea hata kama waliheshimu uamuzi wa mahakama kutupilia nje ombi lao lililolenga kubatilishwa kwa ushindi wa rais Ruto.

About the author

admin

Leave a Comment