Kocha wa Arsenal Mikel Arteta yuko chini ya shinikizo baada ya wakuu wa klabu hiyo kumpa muda wa wiki sita kuandikisha matokeo mazuri la si hivyo atimuliwe.
Baada ya kupoteza mechi mbili za utangulizi ligini kwa kipigo cha 2-0 dhidi ya Brentford na Chelsea mtawaliwa, mashabiki wa klabu hiyo wameanza kumshutumu vikali Mhispania huyo kutokana na mbinu zake za ufundishaji.
Pamoja na presha hiyo ya mashabiki ambao wameanza kwenda uwanjani na mabango kusisitiza apigwe kalamu, mabosi wa klabu nao wamejitokeza na kumpa kocha huyo mechi za kujinasua kwa muda usiozidi wiki sita ili ahepe kutupiwa virago.
Mechi hizo ni pamoja na ya jana Jumatano usiku ya mchujo wa Carabao dhidi ya West Brom ambapo Arsenal ilisajili ushindi wa mabao 6-0 yakifungwa na Pierre-Emerick Aubameyang (3), Nicolas Pépé, Bukayo Saka, na Alexandre Lacazette.
Ipo imani kwamba matokeo mazuri yatarejesha timu hiyo katika nafasi ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.
Leave a Comment