Maafisa wa upelelezi nchini DCI wameanzisha uchunguzi na msako mkali dhidi ya genge la wahalifu sita waliovamia familia moja katika eneo bunge la Bahati kaunti ya Nakuru na kutoweka na mali ya thamani isiyojulikana.
Kulingana na DCI, genge hilo ambalo lilikuwa limejihami kwa panga lilivamia nyumba ya wahasiriwa mida ya saa tatu usiku walipokuwa wanatazama runinga kabla ya kulala.
Majambazi hao walijeruhi mzee mwenye nyumba kabla ya kumfunga mkewe, bintiye, wajukuu watatu na yaya kwa kamba kisha kuanza kupora mali tofuati kwenye nyumba hiyo usiku kucha.
Wahalifu hao wanaripotiwa kufanya uporaji wao kwa zaidi ya saa tisa na kufanikiwa kuiba runinga nne, mitungi mitatu ya gesi, jokofu, kipakatalishi, baiskeli, nguo kati ya vitu vingine.
Vile vile majambazi hao wanasemekana kuhamisha shilingi 80,000 kutoka kwa akaunti ya simu ya binti wa familia na zingine 61,800 kutoka kwa akaunti yake ya benki.
Ni kisa kilichoripotiwa katika kituo cha polisi cha Bahati.
Leave a Comment