MAKALA MAALUM UNAYOWEZA KUYASIKILIZA KWA SAUTI:
Leo tunarejea katika kaunti ndogo ya Rongai, tuangazie kwa mara nyingine mikakati iliowekwa kupigana na ndoa za mapema, na aidha, mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi.
Katika makala tuliokuandalia mwaka wa 2020 na 21 kwa uhisani wa baraza la vyombo vya habari nchini MCK, msikilizaji ulipata kuskia namna kiasi cha wanafunzi 800 na zaidi walivyopata uja uzito wa mapema na wengine kudhulumiwa kimwili punde baada ya shule kufungwa kutokana na kirusi cha Corona.
Kama hukupata kusikiliza makala hayo msikilizaji, utawala wa kaunti ndogo ya Rongai chini ya naibu kamishna msaidizi Ronald Mwiwawi, pamoja na afisa wa watoto Beatrice Mandieka ulisema kati ya mwezi Januari 2020 na Mei 2020, miezi miwili tu baada ya shule kufungwa, kiasi cha visa 520 vya mimba za mapema viliweza kurekodiwa. Mwiwawi alisema matumizi ya dawa za kulevya yaliongezeka sana miongoni mwa wanafunzi, mahusiano haramu yakaongezeka sana miongoni mwao, na wengine wakadhulumiwa na watu walio karibu nao
“Tumeona kwamba matumizi ya bangi, filamu na simu yamechangia katika kuharibu watoto. Utagundua kwamba wengi wanajihusisha na ngono, vijana kwa vijana, japo kuna watu wazima ambao wamehusika na visa hivi vya dhulma. Ila tunawalenga wazazi ambao wametelekeza majukumu yao ya ulezi, tuwafikishe mahakamani wajieleze ni kwa nini hawatimizi majukumu hayo” Mwiwawi akasema
Pia tulizungumza na maafisa wa shirika la Dandelion Afrika, moja kati ya mashirika ambayo yanasaidia kuokoa wanafunzi wanaojipata wakikeketwa, wakiozwa kwa lazima, wakidhulumiwa kimwili au kingono, au wanaopata uja uzito wangali shuleni.
Wendo alisema safari ya kupambana na dhulma za kijinsia na mimba za mapema haijakuwa rahisikwa kuwa visa vingi havikuwa vikiripotiwa. Hii iliwalazimu kuanza kuwafunza wananchi kuhusu dhulma na adhari zake, wakaanza kufunza machifu na maafisa wengine wa utawala kuhusu namna ya kukabiliana na dhulma, na pia wanawekeza ktika miradi ya kiuchumi kukabiliana na umaskini.
“Kwanza tunasaidia wote kutambua dhulma ni nini kwa sababu hapa mashinani akina mama wengi wanaamini kwamba dhulma ni jambo za kawaida. Pia tunawapa mafunzo wazee wa nyumba kumi, machifu, polisi na watawala wote ili wafahamu namna ya kukabiliana na dhulma hizo” Wendo Aszed, mkurugenzi wa Dandelion Afrika.
Licha ya matatizo hayo yote kukumba wanafunzi katika kaunti ndogo ya Rongai, sasa ni dhahiri msikilizaji kwamba angalau, visa hivi vimepungua kufuatia juhudi za pamoja zilizofuata kilio cha wazazi, washikadau kama vyombo vya habari ikiwemo Sauti, baraza la vyombo vya habari nchini MCK, mashirika kama Dandelion Afrika, hazina ya usatawishaji maendeleo NGCDF, machifu, waalimu wakuu kati ya wengine.
Nimepata kuzungumza na afisa anyesimamia fedha kwenye ofisi ya CDF Rongai Henry Koech au Lokirr ambaye amesema ujenzi wa mabweni katika shule za umma ni swala ambalo mbunge wa rongai Raymond Moi alionelea litasaidia kupambana na dhulma hizo. Shule zilizonufaika ni pamoja na ile ya msingi ya Ogilgei, Sasumua, Losibil, Kampi Ya Moto, Setkobor na Chemasis. Kila moja ya bweni hilo limegharimu shilingi milioni 2.5 na linauwezo wa kusetiri vitanda 80.
“Ujenzi wa mabweni hayo ilikuwa moja kati ya ahadi alizotoa mbunge wetu (Raymond Moi) wakati wa kampeni. Hii ilikuwa ni ujenzi wa majaribio kama wazazi watakumbatia mabweni hayo. Lakini imeishia kusaidia kukabiliana na dhulma” Lokirr, afisa wa hazina kwenye CDF ya Rongai akasema.
Lokir anasema baada ya ongezeko la matatizo yaliyokuwa yakiwakumba watoto wasichana haswa kule Soin na Solai, wengi wa watoto hao walijipata waja wazito, na ili kuwaokoa, mabweni zaidi yanahitajika.
“Hii ni mradi ambao umesaidia kukabiliana na changamoto zinazomkabili mtoto wa kike haswa Soin na Solai, ambapo mimba za mapema, kuonzwa mapema na dhulma zingine zimekuwa zikiripotia kwa wingi”.
Ni swala ambalo Wazazi pia wanalifurahia.
Mzazi Susan Mitei anasema “Tunashukuru CDF kwa kujenga bweni la wasichana, masomo imepanda juu, na imeondoa swala la mimba za mapema kwa wanafunzi. Majukumu ya wasichana ni mengi wakikuja nyumbani, lakini wakiwa kwenye shule za bweni, wanapata muda zaidi wa kusoma”.
Wakati uo huo Lokirr anasema serikali ya kaunti ya Nakuru itahitaji pia kuwekeza katika kuchimbia wananchi mabwawa zaidi ya maji, ili kuwaondoa wanafunzi na shuguli za kwenda mitoni usiku ambako wananajisiwa na kudhulumiwa.
“Kuondoa mtoto nyumbani na kumpeleka shuleni ya bweni inamuondolea hatari kubwa. Lengo letu ilikuwa kwanza kuokoa mtoto wa kike kutoka kwa hatari, lakini miradi mingine inahitaji maingilizi pia ya serikali ya kaunti. Kwa sasa kikatiba swala la maji limegatuliwa, hatuwezi kujiingiza kwalo tena” Lokirr akasema
Katika kupambana na dhulma hizi, Lokirr pia anasema swala hili la dhulma limeonekana kwa muda mrefu kama tamaduni, ila jamii inastahili kuachana na hilo na kugeukia maendeleo ya kisasa kama kuelimisha watoto wote pasi na kuzingatia jinsia yao.
“Dhulma zimekuwa zikifanyika kama tamaduni. Lazima tutafute mbinu ya kukabiliana nazo hivi kwamba kila jamii atabadilisha mtizamo, kwa kukumbatia mabweni na kupeleka watoto shuleni” Lokirr amesema
Hata hivyo juhudi hizi hazitoshi. Katika ujumbe wake wa arafa aliotuma kwetu baada ya kuwasiliana naye, mbunge Raymond Moi, anasema mikakati zaidi inahitaji kuwekwa, kwani uchunguzi wao umedhihirisha kwamba baadhi ya wanafunzi wanadanganywa na vijana wachanga kama wale wa boda boda kwa kununuliwa sodo na hivyo wanajipata waja wazito.
Ni swala ambalo Wendo na DCC Mwiwawi wanaunga mkono pia.
“La msingi zaidi ni kulenga wazazi ili kuhakikisha wanatunza watoto wao licha ya umaskini” Mwiwawi akaongeza
Aszed kwa upande wake amesema “Umaskini upo na unaishia kwa wanafunzi kutumwa kufanya kazi ambayo hawakustahili kama kwenda kuchota maji ya kuuza. Wengine wanadanganywa kwamba watanunuliwa sodo na hivyo wanajipata wana wazito au wameambukizwa magonjwa”.
Lokirr hata hivyo anaeleza kwamba pole pole, wazazi wameanza kukumbatia haja ya watoto wao kuwa kwenye mabweni kuliko shule za kutwa.
“Tayari kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi ambao wamejiunga na shule za bweni ambazo tumejenga, na wengi wameonyesha kuongeza kiwango cha elimu kutokana na alama zilizopatikana katika mtihani uliofanywa mwaka huu (2021/2022)” Lokirr ameongeza.
Utafiti wa shirika la data na afya nchini mnamo mwaka wa 2014, unaonyesha kwamba, mmoja kati ya wanafunzi watano walio kati ya mwaka wa 15- wa 19, anapata mtoto au akawa mja mzito nchini. Pia, tahadhari imetolewa kwamba wasichana wasiopungua elfu kumi, hulazimika kuacha shule kila mwaka kutokana na uja uzito wa mapema nchini.
Katika mwaka wa 2020 pekee, wasichana wachanga 330,000 walio kati ya miaka 10-19 walipata uja uzito, miezi kumi pekee tangia shule kufungwa kutokana na corona.
Kinachoshangaza zaidi msikilizaji, ni ripoti ya utafiti wa uchumi mwaka wa 2021 (2021 Economic Survey) iliofanywa na shirika la takwimu nchini KNBS, iliosema wasichana wachanga wapatao 396, 929 walipata uja uzito mwaka wa 2019, na mwaka wa 2020, ikashuka hadi 332, 208, licha ya kwamba washikadau wanaopigana na mimba za mapema wanasema sio hali jhalisi, visa hivi ni vingi zaidi ya inavyokadiriwa.
Kisa na maana, ni kwamba wengi wa waliopata uja uzito wakiwa shuleni, wanakosa kwenda kliniki hospitalini au hata wanaamua kujifungulia manyumbani ili kuficha wanachoita udhalilishaji na fedheha ya umma. Bonyeza hapa kusikiliza makala haya yote.
https://www.sautiyamwananchifm.co.ke/mabweni-kupiga-kumbo-dhulma-na-mimba-za-mapema-na-pius-agata/
Leave a Comment