Muungano wa Azimio la Umoja One–Kenya unayumba huku wanachama wakikosa umoja.
Mrengo huo wa upinzani unaoongozwa na Raila Odinga, umepata pigo kubwa baada ya baadhi ya vyama tanzu kugura na kujiunga na Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais William Ruto.
Lakini kwa sasa duru zinadokeza kwamba Raila anatia kila jitihada ya kuhakikisha kuwa muungano huo hausambaratiki licha ya wanachama wengi kuhama.
Muungano huo ulikuwa na zaidi ya vyama 20 tanzu ulipobuniwa kutumika kama gari la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9
Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wana shauku iwapo Azimio watabuni upinzani mkali wa kukosoa utawala wa rais Ruto.
Mchangauzi wa siasa Martin Oloo anahoji kuwa rasilimali alizo nazo Rais Ruto zitasambaratisha muungano huo na kuleta mkanganyiko katika maeneo ya Nyanza na Magharibi.
Alisema tofauti na Raila, Ruto ni mtu karimu na kuna uwezekano mkubwa kwamba atapenya kuingia maeneo ya Magharibi na Nyanza kama Rais.
Oloo ameongeza kuwa viongozi wa muungano huo hawana maarifa na hivyo watapata aibu zaidi iwapo watajaribu kujipanga upya ili kukabiliana na serikali.
Kauli yake inajiri baada ya aliyekuwa gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambao ni vinara wakuu wa Azimio kutangaza kuwa muungano huo utabuni upinzani dhabiti wa kukosoa serikali ya Kenya Kwanza.
Kalonzo alijifariji kuwa miaka mitano ni kipindi kifupi na kuwataka wafuasi wa Azimio kuuguza majeraha ya kushindwa uchaguzi na kubakia makini.
Makamu huyo wa zamani wa rais alisisitiza kuwa hajakata tamaa ya kuwania urais na kwamba anachukua muda wa kupumzika ili kujipanga upya.
Oparanya naye alidai kuwa wale ambao wamejiunga na Kenya Kwanza walishindwa katika uchaguzi wa Agosti 9 na kuondoka kwao hakutalemaza Azimio.
Leave a Comment