Watu wanaoishi na changamoto za maumbile kwenye kaunti ya Nakuru, wametakiwa kujitokeza kujisajili kama wapiga kura, ili wawe na sauti ya kuchagua viongozi ambao watashughulikia maslahi yao ifikapo mwaka ujao.
Wito huo umetolewa na Omondi Fredrick, mmoja wa viongozi wa kundi la watu wanaoishi na changamoto za maumbile katika kaunti ndogo ya Rongai.
Kulingana na Omondi, wanachama wengi wa kundi lake wameachwa nyuma kimaendeleo kwa sauti zao kupuuzwa na viongozi mashinani.
“Vijana, akina mama na wazee wote wanaoishi na changamoto za maumbile, tujitokeze kule huduma centre tusaidiwe kujisajili kama wapiga kura, ili tuwe na sauti kwenye uchaguzi mkuu na tuachwe kupuuzwa na viongozi” akasema wakati wa mahojiano na kituo hiki kule Kampi ya moto.
Usajili wa wapiga kura bado unaendelea, zoezi hilo likitarajiwa kukamilika Novemba 2, 2021.
Na Miriam Itotia
Leave a Comment