Sports/Michezo

West Ham United wapepeta Aston Villa katika gozi la EPL

West ham united waanza mashambulizi EPL
Written by admin

WEST Ham United walishinda mechi yao ya kwanza msimu huu baada ya Pablo Fornals kuwafungia bao la pekee dhidi ya Aston Villa mnamo Agosti 28, 2022 uwanjani Villa Park.

Bao lililofungwa na Villa katika kipindi cha kwanza halikuhesabiwa na refa baada ya kubainika kuwa mpira wa kona uliopigwa na Lucas Digne ulikuwa umetoka nje kabla ya Ezri Konsa kuujaza wavuni.

West Ham waliimarika katika kipindi cha pili na nusura wafunge bao kupitia kwa Jarrod Bowen aliyemtatiza sana Digne. Hata hivyo, dakika 16 kabla ya mechi kukamilika, Fornals alimwacha hoi kipa Emiliano Martinez na kuvunia West Ham ushindi wa kwanza ligini msimu huu.

Ushindi huo uliowatoa West Ham mkiani mwa jedwali na sasa wanajivunia alama tatu, sawa na Villa. Kichapo hicho kilizidisha presha kwa kocha Steven Gerrard aliyeshuhudia kikosi chake kikizomewa na mashabiki mwishoni mwa kipindi cha pili.

Masaibu ya Gerrard yaliongezwa na jeraha ambalo sasa linatarajiwa kumweka nje kiungo mbunifu Philippe Coutinho kwa kipindi kirefu kijacho.

West Ham walishinda mechi yao saa chache baada ya kukamilisha usajiliwa nyota Lucas Paqueta kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa.

About the author

admin

Leave a Comment