Eli Khumundu, mmoja wa wafanyikazi wa zamani wa mbunge mteule wa Lang’ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o waliodaiwa kumwibia pesa amefunguka kuhusu yaliyojiri.
Katika mahojiano na mwanablogu mmoja Eli ambaye amekuwa akiishi Bungoma tangu tukio hilo alikiri kuwa yeye na mwenzake Morrison Litiema waliiba shilingi milioni moja kutoka kwa moja ya magari ya mtangazaji huyo wa zamani.
“Tulikuwa tumeingia kazi asubuhi kama kawaida. Kuna magari ya mdosi ambayo huwa tunaosha. Ndugu yangu alishika BMW na mimi nikashika Discovery kuosha. Yeye alipata pesa kwa gari ambayo alikuwa anaosha,” Eli alisimulia.
Aliongeza, “Alikuwa anaosha pale ndani akanusa harufu ya pesa. Ata hakuwa amejua iko wapi, alinusa harufu kwanza. Baadaye alichunguza pale ndani na kupata akakuja akaniambia kuna pesa pale,”
Eli alidai kuwa mwanzoni alisitasita kushirikiana na mwenzake kabla ya hatimaye kuingia katika majaribu na kumfuata kutoroka na pesa zile.
Mzaliwa huyo wa Bungoma alimlaumu shetani kwa kitendo hicho chao huku akidai kuwa ilikuwa ni mara yao ya kwanza tu kumuibia bosi wao.
“Huo ni msukumo fulani. Kama sio kutoka kwetu ni kwa kina Morrison. Hatujawahi kuwa na tabia hiyo na hata nimefanya kazi sana hii Nairobi. Kama ningekuwa mwizi sidhani ningekuwa naishi bado. Ningekuwa nimechomwa,” Alisema.
Eli aliendelea kusimulia kuwa baada ya kutoroka na pesa hizo, wasiwasi uliwapanda baada ya Jalang’o kufichua walichofanya na kuanza kuwatafuta.
Alisema kuwa alijuta matendo yake na baada ya wiki moja akapiga hatua ya kumtafuta mwajiri wake kwa simu ili kufanya mikakati ya kuzirejesha pesa zile.
“Tulirudisha pesa. Mimi hakuna hata sumuni moja ambayo nilibaki nayo. Ndio maana mnaona huko nyumbani nateseka,”
Eli ametoa wito kwa Jalang’o kumrejesha kazini huku akieleza kuwa yeye pamoja na familia yake wanateseka sana nyumbani.
Alikiri kuwa kitendo chake cha wizi kilileta taabu nyumbani kwake na hakujawa na amani tangu kilipotokea mwezi Juni.
“Kuna mateso huko nyumbani. Tangu tutoke Nairobi, watoto hawajaingia shule. Bibi aliposikia taarifa hiyo hakuamini kwa vile anapenda mdosi. Hakuna amani. Bibi huwa ananiuliza ni nini hiyo nilifanya. Mpaka anajutia, ndoa yangu iko hatarini, muda wowote bibi anaweza kuenda kwa sababu ya ule upuzi shetani alitufanyisha,” Alisema
Eli amemuomba Jalang’o kumpatia nafasi nyingine ili aweze kuwasomesha watoto wake na kuhudumia familia yake kama ilivyokuwa awali.
Leave a Comment