SERIKALI ya Kaunti ya Baringo imepata amri ya korti ili kuzika miili ambayo haina wenyewe na imekuwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Baringo mjini Kabarnet kwa miezi kadhaa.
Kulingana na supritendanti wa hospitali hiyo Dkt Charles Maswai, zaidi ya miili minane kutoka hospitali ya kaunti ndogo ya Tiaty imekaa katika hifadhi hiyo na kusababisha uhaba wa nafasi kusitiri miili mingine.
Dkt Maswai alisema kuwa mochari hiyo ina uwezo wa kuhifadhi miili 48 pekee na kwa kuwa imekuwa mingi, ile ambayo haijachukuliwa na wenyewe hawapo sasa itazikwa.
“Hifadhi ya maiti ya hospitali hii ilikuwa imejaa ndio maana tukalazimika kuelekea kortini na kupata amri ya kuondoa miili hiyo kisha kuizika. Zaidi ya miili minane katika hospitali ya Tiaty imekaa kwa miezi minane bila kuchukuliwa,” alisema Dkt Mawai.
Hata hivyo, mila na desturi ya jamii ya Pokot inayolazimu miili izikwe siku ambayo mtu amefariki imelaumiwa kwa kuendelea kurundikana kwa miili ndani ya hospitali kadhaa za kaunti hiyo.
Wapokot wanasisitiza kuwa mtu lazima azikwe siku aliyofariki na mahali alikoaga ndiposa wengi wao wanaamua kuiacha miili ya wapendwa wao inayopelekwa kwenye hifadhi ya maiti.
“Pia wanaokaribia au hata kumgusa mtu aliyefariki huchukuliwa kama aliyetiwa najisi. Kwa hivyo, tamaduni inalazimu atengwe kwa siku kadhaa na sherehe hufanyika ya kumtakasa,” akasema Bw Akeno.
Leave a Comment