Tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC, imesimamisha zoezi linaloendelea la usajili wa wapiga kura wapya katika baadhi ya sehemu hapa nchini.
Kuambatana na sehemu ya 5 ya sheria za uchaguzi, tume hiyo kupitia mwenyekiti wake Wafula Chebukati, haitaendesha zoezi la usajili wa wapiga kura wapya katika maeneo ambako chaguzi ndogo zitaandaliwa pamoja na yale ambayo yana kesi mahakamani.
Kwa mujibu wa taarifa ya IEBC, maeneo hayo ni pamoja na wadi ya Nguu/Masumba kaunti ya Makueni ambayo inatarajiwa kuandaa uchaguzi mdogo tarehe 14 mwezi Oktoba mwaka 2021, wadi ya Mahoo CAW katika wadi ya Taita Taveta ambayo itaandaa uchaguzi mdogo tarehe 16 mwezi Disemba mwaka 2021.
Maeneo mengine ni pamoja na wadi Kiagu katika kaunti ya Meru ambapo Mahakama Kuu ilitoa agizo kuzuia tume ya IEBC kuandaa uchaguzi mdogo na eneo bunge la Kiambaa ambapo kuna kesi ya kiuchaguzi inayosubiriwa kuamuliwa.
Hata hivyo mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema mikakati imewekwa kuhakikisha zoezi hilo linaendeshwa katika maeneo hayo punde tu baada ya kukamilika kwa chaguzi hizo ndogo na pia kesi hizo zilizo mahakamani.
Tume ya IEBC ilizindua zoezi la kuwasajili wapiga kura wapya tarehe nne mwezi Oktoba mwaka 2021, na linatarajiwa kudumu kwa siku 30.
Lengo kuu la zoezi hilo ni kuwapa fursa wakenya kujisajili kuwa wapiga kura kote nchini ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022.
Fauka ya hayo wale ambao tayari ni wapiga kura watapata fursa ya kubadilisha maeneo yao ya kupigia kura pamoja na kubadilisha kasoro kuhusu maelezo yao.
Leave a Comment