Wakili Miguna Miguna sasa anasema kuwa tahadhari zinazomzuia kurejea kwake nchini zimeondolewa leo hii Jumatano, kufuatia kuingia mamlakani kwa Rais William Ruto.
Akitumia mitandao ya Kijamii Miguna amesisitiza kwa Wakenya kwamba kukaa kwake uhamishoni kwa muda mrefu kunakaribia mwisho baada ya mkuu mpya wa nchi kuahidi kurahisisha kurejea kwake.
Miguna amesema kuwa ashatayarisha pasipoti yake kabla ya kupanga tarehe ya kusafiri kwake.
Kauli hii inafuatia ahadi ya Rais Ruto ya kutaka Miguna, ambaye alitangaza kumuunga mkono kiongozi huyo wa U.D.A, arejeshwe nchini iwapo angepanda hadi katika afisi ya juu zaidi.
Wakili huyo baadaye alitoa imani yake kuhusu kuruhusiwa nchini baada ya Ruto kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Agosti.
Wakili huyo alifurushwa hadi Kanada 2018 baada ya kushiriki katika hafla ya kuapishwa kwa kinara wa ODM Raila Odinga kama Rais wa Wananchi katika bustani ya Uhuru Park.
Juhudi za kutaka Miguna aruhusiwe kurejea nchini zimekuwa zikigonga mwamba huku wakili huyo akikashifu lawama zilizotolewa na serikali zinazomzuia kusafiri.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani anayeondoka Dkt. Karanja Kibicho hata hivyo alikanusha mara kwa mara kuhusika kwa serikali ya Jubilee katika pingamizi zinazotatiza kurejeshwa kwa Wakili Miguna Miguna nchini.
Leave a Comment