Kaunti ya Baringo ni miongoni mwa kaunti 23 ambazo serikali imetambua kuwa na tatizo la uhaba wa chakula, kufuatia ukosefu wa mvua ya kutosha kwa miaka miwili ambayo imepita.
Akihutubu mjini Mogotio wakati wa hafla ya kusambaza msaada wa vyakula kwa wakaazi wa eneo bunge hilo mnamo Jumanne, msemaji wa serikali kanali mstaafu Cyrus Oguna alisema serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.4 kwa madhumuni ya kusambaza vyakula kwa wakaazi wa kaunti 23 katika kipindi cha mwezi huu wa Oktoba na mwezi ujao wa Novemba.
“Kwa jumla tumeainisha kaunti 23 nchini ambapo kuna upungufu wa chakula. Mwezi wa kumi tumetoa bilioni 1.2, na pia mwezi ujao kiasi sawa na hicho kitatolewa ili kununua chakula cha msaada. ” Oguna alisema.
Katika zoezi hilo la uzinduzi wa chakula cha msaada, kaunti ya Baringo pekee iliweza kupokea jumla ya magunia elfu 47 ya mahindi miongoni mwa vyakula vingine.
“Maharagwe ni maguni 37,400 ya kilo hamsini, mchele magunia 64,100, mafuta katoni 19,500 na magunia mengine 17,500 ambayo yanasheheni chakula cha watoto”, akaongeza Oguna.
Kanali Oguna alisema sekta ya mifugo pia itatiliwa maanani kufuatia uhaba wa maji na lishe, ambao umesababisha vifo kwa idadi kubwa ya mifugo.
na Jeremiah Chamakany
Ni furaha yangu kujumuika nanyi kuendeleza lugha ya kiswahili . Shukrani
Ni furaha yangu kujumuika nanyi kuendeleza lugha ya kiswahili . Shukrani