Serikali ya kaunti ya Nakuru imezindua mpango wa kutoa taulo za hedhi kwa wasichana katika shule zote zilizoko katika kaunti ya Nakuru kwa lengo la kuhakikisha wasichana hao wanasalia shuleni katika siku zao za hedhi.
Kwa mujibu wa waziri wa jinsia kaunti ya Nakuru Silviah Onyango, kila msichna atapokea mfuko ulio na bidhaa hizo na utakaomsukuma angalau miezi minne katika siku hizo za hedhi.
“Ikizingatiwa kwamba janga la virusi vya corona limeumiza wakenya wengi kiuchumi, wazazi wamekwama kifedha kiasi cha kushindwa kuwanunulia wasichana sodo. Mpango huu unalenga kuhakikisha wanafunzi wasichana katika shule zote za msingi za kaunti ya Nakuru wanapokea sodo, ili waweze kusalia shuleni wakati wote” Onyango amesema.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Heshima ilioko Nakuru Magharibi Veronica Ndegwa, kwa upande wake anasema uwepo wa taulo hizo za hedhi utasaidia pakubwa katika kupambana na kuzuia mimba za mapema ambazo huchangiwa na wasichana kupeana miili yao kwa kudanganywa na wanaume waliokomaa kwamba watanunuliwa sodo, na mwishowe wanajipata waja wazito.
Baadhi ya shule zilizonufaika ni pamoja na St Xavier, Baharini, Mogoon, Kaptembwa, na Ngecha miongoni mwa zingine.
Na Sarah Nyangeri Chege
Leave a Comment