Mwanasiasa Koigi Wa Wamwere amesema wapambanaji wa Mau Mau ni watu wa maana katika historia ya Kenya.
Akizungumza mapema leo na runinga moja ya humu nchini, Koigi alisema kuwa licha ya wapambanaji hao wa Mau Mau kuipigania nchi kwa nguvu zao zote,serikali haijawatambua na badala yake kuwasaliti.
Mwanasiasa huyo alisema kuwa si sawa kwa waliopigania nchi kutofurahia matunda ya kazi yao hadi kufikia sasa.
Vile vile alisema baada ya uhuru, viongozi waliochukua usukani walianza kuwa wakoloni weusi na kuleta udikteta zaidi ikilinganishwa na wakati wa ukoloni. Koigi alisema kutokana na hilo uhuru haujaafikiwa kikamilifu.
Kiongozi huyo alisema kuwa sasa huenda kukawa na ukombozi wa tatu hasaa katika siasa za kuwania kiti cha urais.
Aidha, mwanasiasa huyo aliwasuta wanasiasa kwa kuendelea kupiga kampeini licha ya wizara ya afya kuharamisha mikutano ya kisiasa nchini ili kupunguza msambao wa korona.
Leave a Comment