MKENYA Esse Akida ataongoza AC PAOK dhidi ya Rangers katika fainali ya shindano la pili la raundi ya kwanza la Klabu Bingwa Ulaya ya wanawake mjini Thessaloniki, Ugiriki mnamo Agosti 21 saa kumi na nusu jioni.
Wenyeji PAOK walipiga Swansea kutoka Wales 2-0 kupitia mabao ya Eva Vlassopoulos katika nusu-fainali nao Rangers kutoka Scotland wakalemea Ferencvaros kutoka Hungary 3-1 mnamo Agosti 18.
Mshambulizi Akida alikosa nafasi moja nzuri kupitia kichwa chake katika kipindi cha pili. Akida, ambaye yuko katika msimu wake wa pili na PAOK, aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Wanawake ya Ugiriki msimu uliopita aliposukuma wavuni mabao 18.
Katika mahojiano, Akida, 29, alisema kuwa anafurahia kushiriki Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya pili baada ya kuonja dimba hilo msimu uliopita wakati miamba hao wa Ugiriki walizima Agarista Anenii Noi kutoka Moldova 6-0 katika nusu-fainali ya kuingia raundi ya pili kabla ya kupigwa breki na Valerenga kutoka Norway 2-0 katika fainali.
Mshindi kati ya PAOK na Rangers ataingia raundi ya pili ambapo timu zitapigania tiketi za kuingia mechi za makundi.
Leave a Comment