Klabu ya soka ya Arsenal imemtakia afueni ya haraka beki wake Pablo Mari baada ya kushambuliwa jana Alhamisi jioni.
Mari ambaye yuko kwa mkopo katika klabu ya Italia, A.C Monza alikuwa miongoni mwa watu sita ambao walishambuliwa kwa kisu na mwendawazimu mmoja kwenye jumba la maduka katika jiji la Milan jana jioni.
Ripoti kutoka Italia na klabu ya Arsenal zinadokeza kuwa mwanasoka huyo wa Uhispania kwa sasa anaendelea kupata nafuu hospitalini. Mari hata hivyo yuko nje ya hatari kwani alipata majeraha madogo tu.
Shambulizi hilo lilijiri jioni ambapo Wanabunduki walipata kichapo cha aibu dhidi ya P.S.V ya Uholanzi katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Europa. P.S.V ilipiga Arsenal 2-0 katika mechi ya mkondo wa pili.
Arsenal hata hivyo bado wanapewa nafasi kubwa ya kumaliza kileleni mwa kundi A kwani bado wanaongoza wakiwa na alama kumi na mbili. P.S.V inashika nafasi ya pili ikiwa imejizolea pointi 10 kufikia sasa, Bodo/Glimt ni ya tatu ikiwa na pointi nne huku FC Zurich ikishika mkia kwa pointi tatu pekee.
Leave a Comment